Watu waliojenga kwenye maeneo ya upanuzi wa barabara waonywa

Halmashauri ya ujenzi wa barabara mijini imewaonya watu waliojenga mijengo kwenye maeneo ya upanuzi wa barabara mjini Thika kwamba majengo yao yatabomolewa mwezi January mwaka ujao.onyo hilo limetolewa huku serikali inapojiandaa kujenga barabara za safu mbili mjini humo.Wakiongea wakati wa mkutano wa wadau katika mtaa wa Kiangombe mjini Thika, Maafisa wa halmashauri hiyo walisema nyumba zilizojengwa kwenye maeneo ya upanuzi wa barabara zitabomolewa endapo wamiliki wa nyumba hizo hawatazibomoa kwa hiari yao.Afisa mmoja wa halmashauri hiyo ya Kura Josiah Mwangi amesema watatoa ilani kwa wamiliki wa majengo yaliyo kwenye ardhi ya uma.Kulingana na Mwangi, nyumba zinazodaiwa kujengwa kwenye sehemu za upanuzi wa barabara kuanzia British American Tobacco hadi Corner One huko Kiganjo ambako njia ya pembezoni mwa mji huo inakusudiwa kujengwa zitabomolewa.Serikali imetenga shilling billion 1.5 kwa ujenzi wa barabara za safu mbili mjini Thika ambao utaanza mapema mwaka ujao.Awamu ya kwanza itakuwa ujenzi wa barabara ya umbali wa kilomita kumi kutoka barabara kuu ya Garissa kupitia Kivulini, mtaa wa Kisii -Athena-Witeithie hadi Thika Super highway.Awamu ya pili itakuwa ujenzi wa barabara ya umbali wa kilomita 15 kutoka Kenyatta Highway kupitia Munene Industries-UTI-Pilot-Umoja-Kenyatta leather hadi Garissa Road.