Watu 37 Wafariki Baada Ya Mlipuko Wa Bomu Uturuki

Idadi ya wale waliofariki kufuatia shambulizi la bomu la kutegwa ndani ya gari katika jiji kuu la Uturuki, Ankara imefikia watu 37. Waziri wa afya Mehmet Muezzinoglu aliyasema hayo leo akiongeza kusema kuwa watu 71 bado wanapokea matibabu huku 15 wakiwa kaika hali mahututi. Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuwa atakabiliana vilivyo na ugaidi kufuatia kisa hicho cha hivi punde zaidi. Watu 100 walijeruhiwa kufuatia mlipuko huo uliotokea kwenye kituo kikuu cha uchukuzi cha Guven. Mshukiwa mmoja wa shambulizi hilo pia alifariki. Waziri wa maswala ya kitaifa Efkan Ala alisema kwamba uchunguzi utakamilika leo na wale waliohusika kutajwa. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika kwenye shambulizi hilo ingawa duru za serikali zinaibua shaka kuhusu kundi haramu la Kurdistan Workers Party (PKK). Waasi hao wa Kikurdi wametekeleza mashambulizi kadhaa nchini uturuki katika miezi ya hivi maajuzi ambapo mamia ya watu waliuawa baada ya mkataba wa kukomesha vita kumalizika mwaka uliopita.