Watu 16 walazwa hospitali ya Mandera kufuatia mashambulizi Somalia

Raia-16 pamoja na wanajeshi saba wa jeshi la kitaifa la Somalia wamelazwa hospitalini mjini Mandera baada ya kujeruhiwa mapema leo kwenye shambulizi la wanamgambo wa Al Shabaab dhidi ya kituo cha polisi cha Bula Hawa nchini Somalia. Watu kadha wakiwemo wanamgambo wa Al Shabaab yasemekana waliuawa kwenye shambulizi hilo. Wanamgambo hao walikita bendera ya kundi hilo katika kituo hicho cha polisi. Wanajeshi kadhaa wa serikali ya Somalia walikimbilia usalama wao katika kituo cha polisi cha Mandera huku serikali ya KenyaA� ikipeleka maafisa zaidi wa usalama kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili. Kamishna wa kaunti ya Mandera, Frederick Shisia aliyezungumza na shirika la utangazaji la Kenya-KBC kwa njia ya simu amewahakikishia wakazi wa kaunti hiyo na wakenya kwa jumla kuwa maafisa wa usalama wa Kenya wameimarisha doria katika eneo la mpakani.