Watoto 11 Wadungwa Kisu Uchina

Mwanaume mmoja aliyekuwa amejihami kwa kisu aliwadunga visu watoto 11 katika shule moja ya chekechea kusini mwa Uchina na kuwajeruhi vibaya watoto watatu. Mwanaume huyo aliingia katika shule hiyo iliyoko kusini ya eneo la Guangxi Zhuang huku akidai kuwa alikuwa amekuja kumchukua mwanawe. Watoto watatu waliojeruhiwa vibaya walipelekwa kwa matibabu katika hospitali moja ya eneo hilo. Mwanaume huyo anazuiliwa korokoroni. Mwezi Februari mwaka uliopita mvamizi mmoja aliyekuwa na kisu aliwajeruhi watoto kumi katika eneo la Haikou kusini mwa kisiwa cha Hainan kabla ya kujitia kitanzi.