Watatu wakamatwa kwa kulaghai kupitia kadi za simu

Maafisa wa upelelezi hapa nchini wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na visa vya hivi punde vya ulaghai kupitia kadi za simu. Idara ya upelelezi iliwatambua washukiwa hao kama Joseph Kuria Kariuki, Grace Wanjira Mwehia na Meshack Okoth Okuta. Maafisa wa polisi walisema watatu hao walikamatwa kuhusiana na kisa cha hivi punde ambapo mwakilishi wa wadi huko Kiambu alipoteza shilingi milioni 1.9. Maafisa wa polisi wamesema mmoja wa washukiwa wakuu ni afisa mmoja mkuu wa huduma za wateja wa kampuni ya Safaricom ambaye alifutwa kazi. Maafisa wa upelelezi sasa wanafuatilia habari zinazoweza kusaidia kukamatwa kwa watu wengine wawili, mmoja wao akiwa mhudumu wa benki moja ya humu nchini ambako mlalamishi aliweka pesa zake. Maafisa wa polisi wamewahimiza wananchi wakome kutoa habari za kibinafsi kwa watu wasiowajua au kujibu simu au jumbe za watu hao wanaotaka habari hizo.