Washukiwa wa wizi katika benki ya Co-operative wakamatwa

Polisi katika kaunti ya Isiolo wamewakamata washukiwa watano kuhusiana na wizi wa shilingi milioni-26 kutoka benki ya Co-operative mjini Nanyuki hivi majuzi. Aidha, maafisa wa polisi wanamzuilia mmoja wa washukiwa hao kwenye hospitali ya matibabu maalum ya Isiolo baada ya kujeruhiwa kwa risasi wakati wa tukio hilo la wizi. Afisa mkuu wa idara ya upelelezi kaunti ya huko Isiolo, Raphael Barasa amesema washukiwa watatu tayari wameshtakiwa mahakamani ilhali wengine wawili watashtakiwa pindi uchunguzi utakapokamilika. Barasa alisema washukiwa zaidi huenda wakakamatwa kwa kushirikiana na wale ambao tayari wanazuiliwa. Alisema gari linaloshukiwa kununuliwa kwa kutumia pesa zilizoibwa limetwaliwa na kwamba uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo.