Washukiwa Wa Mashambulizi Ya Mpeketoni Yaliyosababisha Vifo Vya Watu 60 Waondolewa Mashtaka

Dereva wa Matatu na mfanyibiashara mmoja waliokuwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 60 ya mauaji kuhusiana na mashambulizi katika eneo la Mpeketoni, kaunti ya Lamu mwaka 2014, wameondolewa mashtaka na mahakama kuu ya Mombasa. Wawili hao Dyana Salim Suleiman, na Mahadi Swaleh Mahadi waliondolewa mashtaka baada ya Justice Martin Muya kuamua kwamba upande wa mashtaka haujadhibitisha bayana kesi inayowakabili. Dyana Salim Suleiman na Mahadi Swaleh Mahadi walitiwa nguvuni kufuatia mashambulizi mabaya katika eneo la Mpeketoni Kaunti ya Lamu, ambapoA� watu 60 waliuawa baada ya kuvamiwa nyakati za usiku. Watu wengine wawili pia waliondolewa mashtaka kumi na mawili ya mauaji kuhusiana na kisa kingine cha uvamizi katika eneo la Hindi; katika Kaunti hiyo ya Lamu. Mahakama ilisema kwamba tuhuma dhidi ya Swaleh ,Auni na Joseph Kimani hazijadhibitishwa. Hii ina maana kwamba watu wanne wameondolewa mashtaka kuhusiana na visa vya uvamizi katika Kaunti ya Lamu.