Washambulizi Wauwa Wafanyanyikazi Wa Shirika La Utoaji Msaada Sudan Kusini

Washambulizi wamewaua wafanyikazi wawili wa shirika la utoaji misaada nchini Sudan Kusini. Wawili hao waliokuwa raia wa nchi hiyo walikuwa wafanyikazi wa shirika la Danish Demining Group na waliuawa walipokuwa wakielekea kazini katika eneo la Yei kusini ya nchi hiyo. Wafanyikazi wapatao 51 wa mashirika ya utoaji misaada nchini Sudan Kusini wameuawa tangu mwezi Disemba mwaka 2013 pamoja na maelfu ya wakazi. Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalizuka nchini humo mwaka 2013 wakati rais Salva Kiir alipomshutumu aliyekuwa naibu wake Riek Machar kwa kupanga njama ya kupindua serikali. Tangu wakati huo taifa hilo limekumbwa na mashambulizi ya kulipizana kisasi lakini matumaini ya amani yameibuka baada ya kiongozi wa waasi Riek Machar kurejea nyumbani kufuatia mkataba wa amani.