Wapiga kura wana hadi alhamisi kudhibitisha maelezo kuwahusu

Wakenya wana siku tatu pekee kuthibitisha taarifa kuwahusu kama vile jina, kituo cha kupigia kura na utambulisho wao kabla ya kukamilika kwa shughuli hiyo siku ya Alhamisi. Shughuli hiyoA� ambayo ilianza tarehe 10 mwezi uliopita ilifaa kufanyika kwa siku 30 kuambatana na sheria ili kuiwezesha tume huru ya uchaguzi na mipaka, (IEBC) kurekebisha sajili ya wapigaji kura na kutilia maanani maswala yoyote ambayo huenda yakachipuza wakati wa shughuli hiyo ya kuthibitisha taarifa za wapigaji kura. Shughuli sawa na hiyo kwa wakenya walio katika nchi za kigeni za Burundi, Rwanda, Afrika kusini, Tanzania na Uganda ilikamilika tarehe 30 mwezi uliopita. Wakenya sasa wanahimizwa kuthibitisha taarifa zao na kurekebisha kasoro zozote ambazo huenda zikawazuia kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu mwezi Agosti. Wakati huo huo leo ni siku ya mwisho ya kuwasilisha kwa tume ya IEBC malalamishi yote yaliyotokana na uchaguzi wa mchujo wa vyama vya kisiasa. Kwenye taarifa mwenyekiti wa IEBCA� Wafula Chebukati alisema kuwa malalamishi yote yanafaa kuwasilishwa kwenye afisi za tume hiyo jijini Nairobi kufikia leo saa kumi na moja jioni. Tume hiyo ilianza kusikiza mizozo iliyotokana na uteuzi huo kuanzia tarehe 4 mwezi huu kwenye mahakama ya Milimani na ilitarajiwa kukamilisha shughuli hiyo leo.