Wanaume wawili wapatikana na ngozi mbili za chui

Wanaume wawili wazee wamefikishwa kwenye mahakama moja ya Kibera kwa kuwa na ngozi mbili za chui za thamani ya shilingi laki-2 kinyume cha sheria. Washukiwa hao wawili walio katika miaka yao ya sitini walikamatwa na maafisa wa shirika la huduma kwa wanyama pori nchini (KWS) kufuatia ripoti za kijasusi. Maafisa hao waliojisingizia kuwa wanunuzi waliwashawishi washukiwa hao kuwapelekea bidhaa hizo zilizopigwa marufuku kwenye uwanja wa michezo wa Nyayo jijini Nairobi. Walikamatwa walipotaka kuwauzia maafisa hao ngozi hizo kwa jumla ya shilingi laki-4. Walishtakiwa kwa kumiliki bidhaa za wanyama pori kinyume cha kifungu 95 cha sheria ya uhifadhi na usimamizi wa wanyama pori. Walikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa thamana ya shilingi nusu milioni kila mmoja.