Wanasiasa Wahimizwa Kujiepusha Na Ghasia

Wanasiasa wamehimizwa kujiepusha na shughuli ambazo huenda zikasababisha ghasia huku nchi hii ikikaribia uchaguzi mkuu mwaka ujao. Askofu Joseph Ntombura, wa kanisa la Kimethodist nchini alizungumzia kuhusu siasa zinazozua ghasia ambazo zinashuhudiwa kwenye baadhi ya maeneo nchini na kutoa wito wa kuvumiliana miongoni mwa viongozi. Akiongea jana wakati wa sherehe ya kufunga kongamano la siku nne la kanisa hilo kwa wanawake katika chuo kikuu cha Methodist mjini Meru askofu Ntombura aliwaonya viongozi dhidi ya kujihusisha na siasa za migawanyiko. Alikariri kwamba kanisa litaendelea kutetea jamii yenye mshikamano ili kuhakikisha nchi hii inasalia na umoja wakati wa kampeni. Alishtumu ghasia zilizoshuhudiwa kwenye baadhi ya maeneo nchini wakati wa sherehe za 53 za siku kuu ya Jamhuri na kutoa wito kwa wakenya kutokubali kutumiwa na wanasiasa kwa manufaa yao ya kisiasa.