Wanariadha Tayari Kuwakilisha Kenya Kwenye Olimpiki

Rais Uhuru Kenyatta leo asubuhi katika Ikulu ya Nairobi atakabidhi bendera ya taifa kwa wanamichezo watakaoiwakilisha nchi hii katika michezo ya Olimpiki mjini Rio de Janiero nchini Brazil ambayo itaanza tarehe 5 mwezi ujao wa Agosti. Chama cha wanariadha humu nchini kimeteuwa timu ya wanariadha 50 wakiwemo wale wa akiba ambao watashiriki kwenye michezo hiyo ya Olimpiki ya mwaka huu mjini Rio. Mshindi mara mbili wa mbio wa marathoni za London Eliud Kipchoge ataongoza timu ya Kenya kwenye michezo ya Olimpiki mjini Rio de janeiro nchini Brazil mwaka huu. Timu hiyo inawajumuisha mabingwa wote wa dunia kutoka hapa nchini wanaojumuisha David Rudisha, Asbel Kiprop, Ezekiel kemboi, Nicholas bett, Julius Yego, Vivian Cheruiyot na Hyvin Kiyeng. Timu ya wanawake itamjumuisha mshindi wa dunia wa nishani ya fedha kwenye mbio za marathoni Helah Kiprop, mshindi wa mbio za marathoni za London Jemima Sumgong na mshindi wa mbio za Marahtoni za Paris, Visiline Jepkesho.