Wananchi Watarajiwa Kutoa Maoni Yao Kuhusu Hukumu Ya Kifo

Wananchi kesho wanatarajiwa kutoa maoni yao kuhusu utoaji hukumu ya kifo na jinsi ya kushughulikia hatia za jinai katika kaunti tano za uliokuwa mkoa wa Nyanza.Maafisa wa kamati kuhusu mamlaka ya kutoa msamaha na ushauri na kituo cha taifa cha kufanya utafiti kuhusu uhalifu wataongoza mjadala wa kutafuta maoni kutoka makanisha, vijana, wanawake, viongozi wa eneo hilo na wananchi kuhusu suala hilo kwa muda wa wiki mbili. Kulingana na katibu mkuu wa kamati hiyo Michael Kagika maafisa wa taasisi hizo mbili watazuru kaunti za Kisii, Nyamira, Siaya, Migori, Homabay na Kisumu. Kagika alisema lengo la mdahalo huo ni kupokea maoni ya Wakenya kuhusu hukumu ya kifo na jinsi hukumu hiyo yaweza kushughulikiwa. Aidha alisema mjadala huo ambao unajiri baada ya kukamilishwa kwa kongamano la sita ulimwenguni la kupinga hukumu ya kifo huko mjini Oslo, Norway, utatoa fursa kwa Wakenya kutoa maoni yao kuhusu hukumu ya kifo na kupendekeza aina ya adhabu ambayo yaweza kutolewa kwa wale wanaokabiliwa na hukumu ya kifo. Kenya ina magereza 118 ambayo yanaweza kuwazuilia wafungwa elfu-26 lakini kwa sasa idadi ya wafungwa ni 52,517 ambapo 32,300 kati yao ni wafungwa wanaotumikia vifungo vyao ilhali wengine 20,217 wanazuiliwa rumande.