Wanamgambo Wanne Wa Al-Shaabab Wauawa Lamu

Wanamgambo wanne wa al-shabaab waliuawa katika mapigano makali na vikosi vya ulinzi vya Kenya KDF baada ya kujaribu kushambulia sehemu ya Milimani karibu na Baure, kaunti ya Lamu. Kulingana na msemaji wa KDF kanali David Obonyo, maafisa wa KDF walipata guruneti ya kurushwa kwa roketi, guruneti mbili za kurishwa kwa mkono, bunduki nne aina ya A�AK 47 na kilipuzi kimoja katika tukio hilo la asubuhi. Kanali Obonyo alisema katika taarifa kwamba mwanajeshi mmoja alipata majeraha katika ufyatulianaji huo wa risasi na anaendelea kupata matibabu. Obonyo alisema wanajeshi wa KDF wanawasaka magaidi hao baada ya kufanya shambulizi dhidi ya kambi ya KDF huko Mangai, kaunti ya Lamu. Aliwahakikishia wananchi kwamba operesheni dhidi ya wanamgambo wa al-shaabab itaendelea hadi magaidi wote waangamizwe kutoka humu nchini ili kuhakikisha kwamba Wakenya wanaendelea kufurahia amani na usalama.