Wanamgambo wa Boko Haram wawauwa wakulima wanne Nageria

Wanamgambo wa Boko Haram wamewauwa wakulima wanne kwenye visa vya urushianaji wa risasi  katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria. Wanamgambo hao waliokuwa wameabiri pikipiki waliwafyatulia risasi wakulima  waliokuwa wakifanya kazi mashambani mwao katika kijiji cha Ngawo Fato Bulamari nje ya mji wa Maidiguri, ambao umekuwa kitovu cha harakati za wanamgambo wa kundi hilo tangu zilipoanzishwa miaka 8 iliopita. Kiongozi wa wakulima hao alisema walipambana na wanamgambo hao kabla hawajatoroka, huku mkulima mmoja aliyedhaniwa kuwa ameuawa akirudi nyumbani. Waathiriwa walikuwa miongoni mwa kundi la wakulima 20 kutoka kijiji jirani waliokuwa wakifanya kazi katika mashamba yao, licha ya kuonywa kuhusu uwezekano wa kushambuliwa na wanamgambo wa Boko Haram. Tangu waanzishe harakati za kutaka kubuni jimbo la kiislamu katika sehemu hiyo takriban raia  20,000  wameuawa, huku wengine milioni  2.6 wakitoroka vijiji vyao tangu mwaka  wa 2009 na kusababisha  mzozo wa  kibinadamu.