Wanamgambo Wa Boko Haram Wauwa Wanakijiji Na Kushika Wanawake Mateka

Wanamgambo wa Boko Haram wamewauwa wanakijiji wanne na kuwashika wanawake watatu mateka karibu na mji wa kaskazini mashariki ya nchi hiyo wa Chibok,ambako miaka miwili iliopita kundi hilo liliwashika mateka na kuwatorosha zaidi ya wasichana 200 wa shule.Wanamgambo hao walikishambulia kijiji cha Kautuva nyakati za alfajiri na kuteketeza nyumba kadhaa na kuwashambulia kwa risasi baadhi ya wakazi wake.Habari hizo ni kwa mujibu wa wakazi wa sehemu hiyo na kundi la wanakijiji wanaosaidiana na wanajeshi kulinda usalama.Kijiji cha Kautuva kipo karibu na mji wa Chibok ambako wanamgambo wa Boko Haram waliwashika mateka takriban wasichana 276 wa shule mnamo mwezi wa Aprili mwaka 2014.Kisa hicho ni sehemu ya harakati za miaka saba sasa za kundi hilo ambalo linanuia kubuni taifa la kiislamu,kaskazini mwa Nigeria. Harakati za kundi hilo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000 nchini humo na kuwafurusha zaidi yaw engine milioni 2 kutoka makazi yao.