Wanafunzi watatu katika shule msingi ya Karura wasombwa na maji

Wanafunzi watatu wa elimu ya chekechea katika shule ya msingi ya Karura, huko Kiambere, kaunti ya Embu walisombwa na mafuriko jana jioni walipojaribu kuvuka mto wa Kiruri. Wanafunzi hao walikuwa katika kundi la watano walipojaribu kuuvuka mto huo uliofurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo. Wanafunzi hao walikuwa wakirejea nyumbani mwendo wa saa kumi alasiri wakati waliposombwa na mafuriko na kuzama. Wana-vijiji walijitokeza na kufanikiwa kuokoa maisha ya wasichana wawili; Ilhali miili ya wengine watatu ilipatikana baadaye mwendo wa saa kumi na mbili jioni. Miili hiyo ilipelekwa kwenye hifadhi ya maiti ya Hospitali ya mafunzo na rufaa ya Embu Level Five. Wazazi wametakiwa kuandamana na wanao wanapoenda shuleni, na pia kufuatilia mienendo yao msimu huu wa mvua ili kuepusha maafa.