Wanafunzi Watano Nyamira Wazuiliwa Katika Korokoro Za Polisi

Wanafunzi watano wa shule ya sekondari ya Nyagokiani katika kaunti ya Nyamira wanazuiliwa katika korokoro za polisi baada ya kukamatwa Jumatano usiku walipojaribu kuteketeza bweni lao. Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo Joseph Mutendei alisema wanafunzi hao walipatikana katika bweni lao na jerikeni iliyojaa petroli. Mutendei alisema waalimu na walinzi waligundua kwamba wanafunzi hao walikuwa wamekwepa masomo ya jioni na walipochunguza, walipatikana ndani ya bweni lao wakinyunyiza petroli tayari kuteketeza beni la shule hiyo.
Wanafunzi hao kisha walikabidhiwa kwa polisi kwa mahojiano. Hivi majuzi, kaunti za Kisii na Nyamira zimekumbwa na msururu wa visa vya kuteketezwa shule. Zaidi ya shule 20 zimeathiriwa na visa vya kuteketezwa mabweni katika kaunti hizo mbili. Kukamatwa kwa wanafunzi hao watano ni ufanisi mkubwa kwa maafisa husika katika kusuluhisha visa vya mara kwa mara vya kuteketezwa shule.