Wanafunzi 62,851 waliofanya mtihani wa kidato cha nne wapata nafasi katika vyuo vikuu vya umma

Wanafunzi 62,851 kati ya zaidi ya laki sita waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana watapata nafasi katika vyuo vikuu vya umma. Waziri wa elimu Amina Mohamed alitangaza haya leo asubuhi katika taasisi ya ustawishaji mtaala humu nchini alipotoa ripoti kuhusu utoaji nafasi kwa wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma.Waziri alisema idadi ya wanafunzi wa kike waliohitimu imeongezeka .

Bi Amina alisema wanafunzi 553 waliohitimu kujiunga na vyuo vikuu wamebadili nia na kuamua kufanya masomo ya stashahada. Aidha alisema wanafunzi 3,619 kati ya wanafunzi 5,747 waliopata alama ya C+ na zaidi hawakupata nafasi katika vyuo vikuu vya umma licha ya kutuma maombi yao. Waziri alihimiza baraza la elimu ya vyuo vikuu vya umma kuwasiliana na wanafunzi hao kuhakikisha wamepata fursa ya kuchagua masomo ambayo wangependa kuendelea nayo hukus kisisitiza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha hakuna mwanafunzi atanyimwa nafasi ya kuendelea na masomo.

Katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, wanafunzi 540,428 ambao ni takriban asilimia 90 ya watahiniwa walipata kati ya alama ya E na C ikilinganishwa na wanafunzi 482,232 waliopata alama hizo mwaka 2016. Idadi ya wanafunzi waliopata alama ya D- pia iliongezeka, hali iliyioibua wasiwasi miongoni mwa wadau.