Wanachama Wa IGAD Waandaa Kikao Cha Dharura Jijini Nairobi

Mawaziri wa mashauri ya kigeni kutoka mataifa wanachama wa shirika la IGAD wameandaa kikao cha dharura jijini Nairobi kutafakari kuhusu mzozo unaokumba Sudan Kusini. Katika taarifa, afisi ya IGAD ilisema kikao hicho kimejiri baada ya mapigano kuzuka upya nchini Sudan Kusini ili kuamua hatua zitakazochukuliwa pamoja na kuwajibisha wahusika.A�Hatua hiyo imejiri huku viongozi duniani wakielezea hofu yao kuhusu kuzuka upya kwa ghasia nchini Sudan Kusini. Hapo jana, msemaji wa ikulu, Manoah Esipisu alisema rais Uhuru Kenyatta amezungumza na rais Salva Kiir na kumhimiza yeye pamoja na aliyekuwa kiongozi wa waasi, Riek Machar kuchukua hatua za haraka kurejesha amani mjini Juba. Kenya ilitekeleza wajibu mkubwa katika kuafikia mkataba wa amani baina ya Kiir na Machar na hivyo imesikitishwa na kuzuka upya kwa ghasia nchini humo. Zaidi ya watu-150 wameripotiwa kuuawa kufuatia mapigano yaliyoanza ijumaa, huku vyombo vya habari nchini humo vikisema huenda idadi hiyo imefikia watu-270. Mapigano hayo ndiyo ya kwanza kati ya jeshi na waliokuwa waasi mjini Juba tangu Machar alipotwaa wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais, baada ya mapigano ya miaka mitatu yaliosababisha vifo vya maelfu ya watu.