Walioshinda mchujo wa Jubilee wapokea vyeti vya uteuzi

Chama cha Jubilee kimeanza kutoa vyeti vya uteuzi kwa takriban wagombeaji-1,900 walioshinda kwenye mchujo wa chama hicho. Katibu mkuu wa chama cha Jubilee, Raphael Tuju amesema vyeti hivyo vinatolewa katika kaunti kuanzia leo. Tuju amewahakikishia wawaniaji kwamba vyeti hivyo ni halali. Tuju amesema vyeti hivyo vina nambari maalum ambazo zitazuia visa vya kughushi. Aidha nambari za vyeti hivyo zitawasilishwa kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka. Wakati huo huo Tuju amesema rufaa-529 ambazo zilikuwa zimewasilishwa kwa jopo la kushughulikia mizozo ya vyama vya kisiasa zimeshughulikiwa na uamuzi utatolewa jumapili ijayo. Tuju amesema makarani elfu-45 kati ya elfu-60 waliosimamia mchujo wa chama cha Jubilee wamelipwa kwa njia ya M-Pesa.