Mbadi ataka makamishna waliosalia kwenye tume huru ya uchaguzi na mipaka kuondoka mara moja

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha ODM John Mbadi amesema makamishna waliosalia kwenye tume huru ya uchaguzi na mipaka wanapaswa kuondoka mara moja. Mbadi alisema upinzani umekuwa ukihoji tume ya IEBC, akiongeza kwamba usimamizi wake unapaswa kupangwa upya.

Alidai wakenya wameghadhabishwa na jinsi makamishna hao watatu walivyojiuzulu siku ya jumatatu huku akisema marekebisho katika tume hiyo yanapaswa kuangaziwa kwenye mdahalo wa kitaifa.

Kwingineko katibu mkuu wa chama cha ODM, Edwin Sifuna ameitaka serikali izindue kikao cha wadau kisichoegemea upande wowote kusimamia kubuniwa kwa tume hiyo ili wakenya wawe na imani na uwezo wake kusimamia chaguzi siku za usoni.

Sifuna alisema kujiuzulu kwa tume hiyo kunathibitisha hofu ya chama cha ODM kuhusu maovu katika tume hiyo. Alisema majadiliano yoyote kuhusu kubuniwa kwa tume hiyo yanapaswa kuhusisha mazungumzo kuhusu kubuniwa kwa usimamizi wake.