Waliokuwa Viongozi Wa Wanafunzi Chuo Kikuu Cha Nairobi Wataka Uchaguzi Ufutiliwa Mbali

Baadhi ya waliokuwa viongozi wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi wamewataka wasimamizi wa chuo kikuu hicho kufutilia mbali uchaguzi wa hivi majuzi wa chama cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi-SONU wakidai ulikumbwa na ghasia na udanganyifu kumpendelea Babu Owino na washirika wake. Kundi hilo likiongozwa na Moses Oburu lilidai kuapishwa haraka kwa Babu Owino ni wa kushukiwa na unakiuka katiba ya chama cha SONU, ambayo inahitaji kiongozi wa wanafunzi aliyechaguliwa kuapishwa hadharani wiki moja baada ya uchaguzi. Oburu alisema viongozi wa wanafunzi wenye malalamishi sharti washughulikiwe kwa usawa na wasimamizi wa chuo kikuu. Wakati huo huo, waliokuwa viongozi wa wanafunzi wamewataka wasimamizi wa chuo kikuu cha Nairobi kubuni kamati itakayowajumuisha waakilishi wa wanafunzi kutoka mabewa yote ya vyuo vikuu. Kamati hiyo itajukumiwa kuchunguza upya katiba ya chama cha SONU ikiwa ni pamoja na kujumuisha vifungu ambavyo vitaweka muda wa kuhudumu wa kiongozi wa wanafunzi.

 

A�