Walimu watishia kugoma

Katibu mkuu wa chama cha kitaifa cha walimu hapa nchini  KNUT Wilson Sossion ametahadharisha kuwa walimu huenda wakalazimika kugoma ili kuzuia tume ya kuwaajiri walimu TSC kutekeleza sera mpya za kuwahamisha walimu wakuu kutoka shule moja hadi nyingine na pia swala la kutathmini utendakazi wa walimu . Sossion amesema mgomo huo huenda ukaanza mwezi Septemba. Akiongoza karamu ya kuwaaga walimu wawili katika shule ya msingi ya Ekige huko  Borabu, Sossion alishinikiza sera hizo ziondolewe na tume hiyo iwaombe walimu msamaha. Alisema sera hizo zinaumiza na ni hatari kwa taaluma ya elimu hapa nchini. Mwekahazina wa kitaifa wa chama hicho John Matiang’i alikashifu  pendekezo la kuwa na sare zinazofanana katika  shule zote hapa nchini akisema pendekezo hilo halina manufaa yoyote katika kuboresha matokeo ya mitihani shuleni.