Walimu Wahimizwa Kuwatayarisha Wanafunzi kwa Mtaala Mpya Wa Elimu

Walimu wamehimizwa waanze kuwatayarisha wanafunzi kwa mtaala mpya wa elimu uliopendekezwa humu nchini. Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na naibu wa mkurugenzi wa Elimu Martin Orwa katika shule ya sekondari ya wasichana ya Kathiani katika kaunti ya Machakos, Waziri wa Elimu Fred Matianga��i alisema serikali imeanzisha shughuli ya kuupitia upya mfumo wa elimu wa 8-4-4 ambao umetumika humu nchini kwa miongo mitatu ili kuratibu mfumo wa elimu humu nchini kuambatana na mahitaji ya karne ya 21. Chini ya mtaala mpya uliopendekezwa wa 2:6:6:3 serikali inapendekeza wanafunzi kumaliza miaka miwili ya elimu ya chekechea, miaka sita katika elimu ya msingi, miaka mingine sita katika elimu ya sekondari na miaka mitatu katika elimu ya chuo kikuu. Hata hivyo, elimu ya sekondari itagawanywa kuwa elimu ya sekondari ya chini na ya juu.