Wakurugenzi wa Kenya Power Waachiliwa kwa dhamana

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Kenya Power aliyesimamishwa kazi Ken Tarus pamoja na maafisa wengine kumi wakuu wa kampuni hiyo wanaokabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ufisadi kutokana na ununuzi wa mitambo duni ya transfoma katika kampuni hiyo wameachiliwa kwa dhamana. Hakimu mkuu wa mahakama ya kukabiliana na ufisadi Douglas Ogoti aliwaagiza kulipa bondi ya shilingi milioni tatu au dhamana ya shilingi milioni moja pesa taslimu kwa sharti kuwa watakabidhi mahakama hati zao za usafiri na kuripoti kwenye afisi za idara ya ijasusi kila baada ya majuma mawili. Akiwapa dhamana hiyo, Ogoti aliamua kwamba hakuna ushahidi wa kutosha uliowasilishwa mahakamani kubainisha uwezekano wa washukiwa hao kuingilia mashahidi iwapo wataachiliwa kwa dhamana. Mahakama hiyo hiyo ilitoa agizo kuwataka wakurugenzi wawili wa kampuni ya M/S Muwa ambao hawakufika mahakamani kwa misingi kuwa walikuwa wamesafiri nje ya nchi kufikishwa mahakamani. Upande wa mashtaka ulikuwa umeiomba mahakama itoe agizo la kuwakamata wawili hao ikidai kwamba wanakwepa haki. Kikao cha kuratibu masharti ya kesi hiyo kitaandaliwa tarehe 6 mwezi ujao.