Wakulima wa mahindi wanamasikito, NCPB kuagiza mahindi kutoka nchi jirani

Wakulima wa mahindi katika eneo la North Rift wameelezea masikitiko yao kuhusiana na hatua ya halmashauri ya mazao na nafaka nchini (NCPB) ya kuagiza mahindi kutoka nchi jirani ya Uganda. Akizungumza na wanahabari mjini Eldoret, mkurugenzi wa chama cha wakulima nchini, A�Kipkorir Arap Menjo, amesema hatua hiyo imewaathiri wakulima huku wakilazimika kuuza mazao yao kwa mawakala kwa bei duni. Vile vile, Menjo alilalamikia huduma duni wanazopata wakulima kutoka kwa halmashauri hiyo wanapowasilisha mahindi yao kwenye maghala yake. Alisema kuwa wakulima hulazimika kusubiri kwenye foleni hata kwa juma moja bila kuhudumiwa hali A�ambayo inahatarisha mazao yao. Mkurugenzi huyo ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha inawalipa wakulima hao mara tu wanapowasilisha mazao yao akisema kuwa mara ya mwisho wakulima hao walipokea malipo ni katikati ya mwezi uliopita.