Wakulima wa mahindi Pokot Magharibi na Trans-nzoia walalamikia mrundiko wa mahindi kutoka nchi jirani

Wakulima wa mahindi katika kaunti za Pokot Magharibi na Trans-nzoia wamelalamika vikali kuhusu mrundiko wa mahindi ya bei ya chini kutoka taifa jirani la Uganda, jambo ambalo limewapokonya soko wakulima wa eneo hilo.  Aidha, wakulima hao wamekashifu serikali kwa kuto-shughulikia changamoto zinazokumba sekta ya kilimo ambazo zimesababisha kushuka kwa bei ya mahindi.

Gavana wa Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo amesema wakulima wengi katika eneo hilo wameamua kupanda mimea mingine kwani bei ya sasa ya mahindi ni shilingi mia nane kwa gunia la kilo-90. Prof Lonyangapuo amelaumu serikali ya kitaifa kwa kuto-wakinga wakulima wa humu nchini dhidi ya mashindano yasiofaa.

Kwingineko, wakulima wa majani chai katika kaunti ya Kericho wametoa wito kwa serikali ya kitaifa kuvunja kampuni ya KTDA kwa sababu ya usimamizi mbaya. Wakiongozwa na William Ketien, wakulima hao wamesema wamewasilisha barua kadhaa kwa kampuni ya KTDA na serikali wakitaka kampuni ifanyiwe marekebisho lakini hakuna lolote lililojiri.

Wakati huo huo, zaidi ya wakulima-700 katika eneo la Sosoni, katika kaunti ndogo ya Magarini sasa wanaweza kupata mikopo kutoka kwa serikali na taasisi nyingine za kifedha baada ya kukabidhiwa hati za usajili na kundi la Anglican Development Services, jambo ambalo litawawezesha kuimarisha hali yao ya maisha