Wakristo Wakusanyika Kuadhimisha Pasaka

Wakristo kote nchini jana walikusanyika makanisani kuadhimisha kufufuka kwa Yesu kristo. Na kwenye kanisa la All saints Cathedral jijini Nairobi, Askofu mkuu wa kanisa la Kianglikana Eliud Wabukhala, alihubiri ujumbe wa amani, kutubu, kusameheana na maridhiano. Kadhalika aliwahimiza viongozi waliohusishwa na ufisadi kusalimisha rasilmali za serikali. Na kwenye kanisa la Gospel Assemblies mtaani South B, Askofu Gerry Kibarabara alitoa ujumbe sawa na huo. Na jijini Vatican, Baba Mtakatifu Francis aliongoza misa ya Jumapili ya Pasaka chini ya ulinzi mkali iliyohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye uwanja wa St. Peter’s. Kwenye ujumbe wake wa Pasaka, Papa Francis aliuhimiza ulimwengu kutumia silaha ya upendo kukabiliana na uovu wa ukatili kufuatia mashambulizi yaliyotekelezwa jijini Brussels, ubelgiji. Baadaye kwenye ujumbe wake wa mara mbili kwa mwaka kwa jiji hilo na ulimwengu kwa jumla alizngumzia ghasia, ukosefu wa haki na vitisho kwa amani katika sehemu nyingi duniani. Alitaja mashambulizi yaliyotekelezwa hivi maajuzi nchini ubelgiji ambapo takriban watu 31 waliuawa na wanamgambo wa kiislamu na pia yale yaliyotekelezwa nchini uturuki, Nigeria, Chad, Cameroon, Ivory Coast, na Iraq. Papa mwenye umri wa miaka 79 ambaye ni raia wa Argentina aliwahimia watu kutumia matumaini ya Pasaka kushinda uovu unaoyakumba maisha ya watu wengi duniani.