Wakili akosoa mpango wa kuapisha Raila

Wakili  mmoja wa hapa jijini  Nairobi ametaja tangazo la hapo jana  la kiongozi wa  Muungano wa NASA  Raila Odinga kwamba ataapishwa kuwa Rais kama tamko la kisiasa lisiloungwa mkono kisheria.  Wakili James Mamboleo  alisema  matamshi kama hayo sio mema kwa nchi kwani yanaweza kuchangia vurumai.  Kulingana na Mamboleo, katiba imebaini wazi kuhusu nani anafaa kuapishwa kuwa rais na haitoi fursa ya marais wawili kuapishwa kuongoza nchi moja.

Mamboleo anasema kuwa Raila Odinga ambaye alihusika kwa kina katika kutayarisha katiba mpya ya mwaka  2010 anastahili kuwa msitari wa mbele katika kuitii. Mamboleo  anahoji kuwa Wakenya wanafaa kutii katiba hata kama inakwenda kinyume cha maslahi yao ya kibnafsi.  Alisema kufuatia kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta hapo jana, taifa hili linafaa kuzingatia maswala mengine baada ya kipindi kirefu cha uchaguzi.  Mamboleo alikuwa akitoa maoni kuhusu  taarifa iliyotolewa jana  na kiongozi wa upinzani kwamba ataapishwa kuwa rais tarehe  12 mwezi ujao.