Wakenya waadhimisha siku ya kuwakumbuka waathiriwa wa ajali za barabarani

Wakenya waliungana na dunia katika kuadhimisha siku ya kuwakumbuka waathiriwa wa ajali za barabarani waliopoteza maisha yao kwenye ajali hizo. Akiongea katika sehemu ya Karai huko Naivsha, gavana wa kaunty ya Nakuru Lee Kinyanjui alisema serikali yake itashirikiana na wizara ya uchukuzi ili kuhakikisha hatua zote za kuhakikisha usalama barabarani zinaungwa mkono. Katika kaunty ya Taita Taveta halmashauri ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani ikishirikiana na polisi wa Trafiki, chama cha msalaba mwekundu na kile cha wamiliki wa matatu huko Voi waliadhimisha siku hiyo kwa kuandamana kutoka Caltex Voi hadi kituo cha mabasi cha Voi ambako walikusanyika kwa majadiliano kuhusu masuala ya usalama barabarani. Maafisa wa NTSA walitumia fursa hiyo kuwaeleza madereva wa magari jinsi vifaa vya kupima kiwango cha ulevi vinavyofanya kazi. Siku hii huadhimishwa jumapili ya tatu ya mwezi Novemba kila mwaka. Ni siku ambapo pia watu huyashukuru mashirika ya kutoa huduma za dharura na kutafakari kuhusu mzigo na gharama ambazo hutoklana na mikasa hiyo. Miaka miwili iliyopita serikali za mataifa ya dunia zilianzisha harakati za kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani ifikapo mwaka 2020.