Wakenya Wasubiri Hotuba Ya Rais Kenyatta Kwa Hamu

Wakenya wanasubiri kwa hamu hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta kwa taifa hapo kesho ambayo wengi wanatarajia itazingatia kile ambacho serikali imefanikisha katika muda wa miaka mitatu tangu ichukue hatamu za uongozi. Hayo ndiyo matarajio huku kiongozi wa walio wengi katika bunge la taifa Adan Dualle akigusia kwamba hotuba hiyo pia itazingatia umuhimu wa ziara za rais huko nga��ambo kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii. Wakati wa hotuba ya Rais kwa taifa mwaka uliopita Rais Kenyatta aliangazia kuhusu ufisadi na akatoa orodha ya watu waliotajwa na tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi (EACC) wakiwemo mawaziri kwa bunge ili wachunguzwe. Maafisa kadhaa wa ngazi ya juu serikalini wakiwemo mawaziri sita na makatibu kadhaa wa wizara waliachishwa kazi. Katiba inaeleza kwamba kiongozi wa taifa atatoa taarifa kila mwaka katika bunge kuhusu usalama wa taifa, ufanisi wa nchi katika kutimiza majukumu yake ya kimataifa na kiwango ambacho nchi inaendelea kudumisha maadili yake ya kitaifa na kuendeleza malengo yake ya utawala.