Wakenya wanawiri kwenye mchezo wa tenisi

Wachezaji wa Kenya walionesha mchezo wa kuridhisha katika mashindano ya tenisi ya BNP Paribas kwa wachezaji walemavu wanaotumia viti vya magurudumu katika uwanja wa kilabu cha Nairobi, huku timu ya akinadada ikitwaa ubingwa nayo ya wanaume ikimaliza katika nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo yaliyoanza juma hili na kumalizika jana.

Timu ya akinadada ilimakinika katika awamu ya nusu fainali na kujikatia tiketi ya fainali ambapo iliishinda Tanzania na kutwaa ubingwa. Kwenye fainali dhidi ya Tanzania, Kenya iliishinda mechi ya kwanza seti za 6-3, 6-2 kisha ikalemewa mechi ya pili 3-6, 6-3, 3-6. Lakini wenyeji hao walitawala mchuano wa tatu na kushinda seti mbili kwa bila za 6-2, 6-2 na kuibuka washindi. Wenzao wa kiume walikuwa na kibarua kigumu nusu fainalini ambapo walishindwa na kujipata katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu. Kwenye awamu hiyo ya kuwania nafasi ya tatu, Kenya iliishinda Tanzania mechi tatu kwa bila. Kenya ilishinda mechi mbili kwa seti za 6-3, 6-2 na 6-0, 6-0 kabla ya kutoka nyuma katika mechi ya tatu na kushinda seti mbili kwa moja za 3-6, 6-4, 6-2. Morocco ilitwaa ubingwa wa wanaume kwa kuishinda Misri fainalini.