Wasafiri kulipa shilingi 700 kutoka Mombasa hadi Nairobi

Wakenya sasa watalipa shilingi 700 katika daraja yaA� economy kusafiri baina ya Mombasa na Nairobi kufuatia uzinduzi wa treni ya kubebea abiria itakayosafiria kwenye reli ya kisasa na rais Uhuru Kenyatta. Akiongea wakati wa uzinduzi wa treni ya kubeba abiria mjini Mombasa, rais Uhuru Kenyatta alisema treni hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa muda unaotumiwa kusafiri kati ya miji hiyo miwili. Aidha rais alisema treni hizo zitaimarisha sekta ya utalii hapa nchini. Wakati huo huo, rais aliwahimiza Wakenya kutolalamika kuhusu changamoto zinazokumba reli hiyo katika siku hizi za mwanzo akisema ni za kawaida. Aliwakosoa viongozi wa upinzani kwa kupinga miradi ya maendeleo ya serikali akisema hawana nia ya kuona taifa hili likisonga mbele. Rais Kenyatta aliwataka Wakenya kuungana kujenga taifa hili.Kwa sasa rais Kenyatta amejiunga na Wakenya wengine wanaosafiri kwa treni hiyo kwa mara ya kwanza kutoka Mombasa hadi jijini Nairobi. Treni hiyo al-maarufu Madaraka Express inaweza kubeba abiria 1,260.