Wakazi Wa Pwani Wahimizwa Kugura Upinzani Na Kujiunga Na Mrengo Tawala Wa Jubilee

Wakazi wa eneo la Pwani wamehimizwa kugura upinzani na kujiunga na mrengo tawala wa Jubilee. Waziri wa ugatuzi Mwangi Kiunjuri aliyezuru eneo hilo akiandamana na baadhi ya viongozi wa serikali aliwambia wakazi hao kuwa wanapaswa kujiunga na mrengo wa Jubilee ili wawe kwenye serikali ijayo. Akiongea katika kambi ya chifu ya Mwangulu huko Lungalunga katika kaunti ya Kwale ambako alitoa msaada wa chakula kwa wakazi hao, Kiunjuri alisema serikali ya Jubilee inajitahidi kushughulikia changamoto zinazokumba wakazi wa eneo hilo. Alimhimiza gavana wa Kwale, Salim Mvurya kujiunga na viongozi wengine wa eneo la Pwani ambao wameeleza azma ya kushirikiana na serikali.

Maoni ya Kiunjuri yaliungwa mkono na waziri wa madini Dan Kazungu ambaye alisema uteuzi wake ni ishara tosha kuwa serikali ya Jubilee inajali maslahi ya wakazi wa Pwani.