Wakaazi Wa Vihiga Kukosa Huduma Za Kaunti Wasipojisajili

Serikali ya kaunti ya Vihiga imewahimiza wakaazi kujisajili kama wapiga kura ili waweze kupata huduma za serikali. Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC inalenga kusajili kati ya wapiga kura milioni nne na sita kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao. Gavana wa kaunti ya Vihiga Moses Akaranga ameagiza idara zote katika kaunti hiyo kuthibitisha iwapo wakaazi wanaotafuta huduma za serikali wamejisajili kuwa wapiga kura. Kwenye arafa, Akaranga hata hivyo amesema ni wagonjwa wanaotafuta huduma za matibabu ambao watashughulikiwa bila sharti hilo. Maafisa katika kaunti hiyo wanahitajika kuhakikisha wale wanaotafuta huduma wanatuma nambari zao za vitambulisho vya kitaifa kwa nambari 22464 A�ili kuthibitisha usajili wao huku viongozi wote wa kisiasa wakiimarisha juhudi za kuhakikisha wakenya wamejisajili kuwa wapiga kura.