Wakaazi Wa Kirinyaga Wamtaka Gavana Awajibikie Matumizi Ya Bilioni 3.4

Wakazi wa kaunti ya Kirinyaga waliandamana kutaka gavana Joseph Ndathi awajibikie matumizi ya shilingi bilioni 3.4 zilizotengwa katika bajeti ya kaunti hiyo. Wakazi hao walichukua hatua hiyo kufuatia taarifa ya mkaguzi mkuu wa mahesabu, Edward Ouko kuashiria kwamba kaunti hiyo haijaelezea kikamilifu jinsi pesa hizo zilivyotumiwa katika kipindi cha kifedha cha mwaka 2014/2015. Wakazi hao waliofunga barabara walisababisha msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara kuu ya Sagana kuelekea Karatina mjini Sagana, walisema miundo msingi katika kaunti hiyo ni mbovu wakishangaa jinsi pesa zilizotengewa miradi ya aina hiyo zilivyotumiwa, ilhali wizara ya fedha hutenga pesa za kufadhili maendeleo. Kundi hilo limesema limemwandikia gavana barua ajiuzulu kusuburi matokeo ya uchunguzi na kwamba tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi iingilie kati ili kuchunguza swala hilo.