Waititu awasilisha kesi mahakamani dhidi ya IEBC

Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu amewasilisha kesi mahakamani kutafuta maagizo ya kushurutisha tume huru ya uchaguzi na mipaka- IEBC kuandaa uchaguzi mpya wa urais tarehe 26 mwezi huu kama ilivyopangwa. Kwenye ombi lake, Waititu amedai kwamba kuchelewa kwa uchaguzi kutaathiri uchumi. Akiongea baada ya kuwasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu ya Kiambu, Waititu alisema wakenya wamechoshwa na wasiwasi uliopo kutokana na kujiondoa kwa mgombeaji wa NASA, Raila Odinga kwenye kinyanganyiro cha urais. Aidha Waititu alisema anaunga mkono kikamilifu marufuku ya maandamano ya muungano wa NASA katika miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu iliyotangazwa na waziri Matiangi aliyesema uharibifu wa mali ulioshuhudiwa hauwezi kuruhusiwa uendelee.