Waislamu kote nchini wazidi kusherekea siku kuu ya Idd ul Fitr

Waislamu kote nchini walisherehekea siku kuu ya Idd ul Fitr, kuashimisha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa sala na sherehe. Maelfu ya waliungana na waumini wenzao katika sehemu nyinginezo za ulimwengu kuadhimisha moja ya siku muhimu katika kalenda ya waislamu. Hapa jijini Nairobi, maelfu ya waislamu huko Kibera walifanya sherehe za EID na wakaahidi kuzingatia amani na jamii nyingine zinazoishi huko Kibera. Hayo yamejiri huku kukiwa na hofu miongoni mwa jamii ya wanubi kwamba hati ya kumiliki ardhi walizopewa na rais Uhuru Kenyatta huenda zikawabagua jamii nyingine zilizoishi huko Kibera kwa miaka mingi.Kwingineko mamia ya waumini wa kiislamu walikusanyika katika uwanja wa Sir Ali Muslim katika eneo la Park road na sehemu za Ngara, Eastleigh, South B, South C na nyinginezo jijini Nairobi kwa sala na sherehe za kuadhimisha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Huko Mombasa, Kadhi mkuu Sheikh Ahmad Muhdhar aliwaongoza waumini katika sala katika uwanja wa michezo wa kaunti ya Mombasa ambako alitoa wito kwa watu kuishi pamoja kwa amani miongoni mwa wakenya wote. Sheikh Mohammad Dor alitoa wito kwa waislamu washiriki walicho nacho na wasiobahatika kuambatana na imani ya kiislamu.