Wahudumu Wa Afya Wanaosababisha Vifo Kiholela Kuadhibiwa

Waziri wa afya Dkt . Cleopas Mailu jana alilalamikia ongezeko la utepetevu katika hospitali na kusema unasabisha aibu na unapaswa kukomeshwa. Waziri huyo aliyekuwa akiongea katika warsha ya mashauriano ya wadau jijijni Nairobi, alishtumu madai ya utepetevu unaohusishwa na vifo vya hivi majuzi katika vituo vya afya na kutoa wito kwa madaktari na wauguzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao. Waziri huyo alitoa wito kwa bodi za uthibiti kama ile ya matibabu kuimarisha utendakazi wake katika kuhakikisha kuwa maafisa wa afya wanaosababisha vifo kupitia utepetevu wanachukuliwa hatua. Alionya kuwa kila mhudumu wa afya atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua za kinidhamu kupitia taasisi husika. Akigusia hofu ya kikosi cha Kenya kinachoelekea RIO kuwa huenda kikawa katika hatari ya maambukizo ya virusi vya ZIKA, waziri huyo aliondoa hofu kwa kusema kuwa wamechukuwa hatua mwafaka za kuhakikisha usalama wa wakenya hao.