Wahome kuzikwa nyumbani kwake kesho

Aliyekuwa Gavana wa Nyeri marehemu  Wahome Gakuru atazikwa kesho nyumbani kwake    katika sehemu  ya Kirichu, eneo bunge la Nyeri mjini. Zaidi ya  waombolezaji alfu 30 wanatarajiwa kuhudhuria  ibada ya mazishi.  Kulingana na Afisa mkuu wa Maswala ya  Miundo msingi katika kaunti ya Nyeri, Muthui Kariuki, Rais  Uhuru Kenyatta,  naibu wake William Ruto  na mawaziri kadhaa  watahudhuria ibada  ya  mazishi itakayofanyika katika uwanja wa shule ya upili   ya wavulana ya Kagumo. Maandalizi  ya mazishi ya marehemu gavana Gakuru yanaongozwa na kamati tatu  katika kiwango cha serikali ya kitaifa, serikali ya kaunti na pia familia yake.   Waziri wa  Habari na   Teknolojia ya Mawasiliano  Joe Mucheru anaongoza kamati ya serikali ya kitaifa jijini Nairobi  huku Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga akiongoza kamati ya  kaunti. Gakuru aliaga dunia wiki mbili zilizopita  kwenye ajali ya barabarani  baada ya kuhudumu kwa miezi mitatu tu.   Alikuwa na umri wa miaka  51 na amemwacha mjane Catherine Gakuru na watoto watatu wa kiume.