Wahadhiri wasisitiza mgomo utaendelea

Viongozi wa chama cha wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma wanasisitiza kuwa mgomo wao unaendelea kwani hawajapata majibu kuhusu malalamishi waliyoyasilisha kwa wizara ya elimu hapo jana. Akiongea an shirika la KBC, naibu mwenyekiti wa chama hicho, Prof Joseph Mberia alipuuzilia mbali taarifa ya mwenyekiti wa baraza la pamoja la ushauri la vyuo vikuu, Prof Paul Kanyari iliyowahimiza wahadhiri kutosheka na shilingi bilioni-4.7 zilizotolewa na serikali kugharamia nyongeza yao ya mshahara na marupurupu. Mberia alisema taarifa hiyo ilipuuza juhudi za wahadhiri hao kudai haki yao. Alitoa wito kwa rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati ili kukomesha mgomo huo. Vyama vya wahadhiri na wafanyikazi wengine wa vyuo vikuu vinalalamika kuhusu kutolewa kwa sehemu ya pesa walizopasa kulipwa kuambatana na mkataba kati yao na serikali na wanataka mkataba huo utekelezwe kikamilifu. Masomo yamelemazwa katika vyuo vikuu vya umma huku mgomo huo ukiingia siku ya tano.

A�