Wagonjwa Wataabika Kufuatia Mgomo Wa Madaktari

Wagonjwa wanaendelea kutaabika hospitalini huku mgomo wa madaktari ukiingia mwezi wa tatu bila matumaini ya kupatikana kwa suluhisho. Maafisa wa chama cha madaktari pamoja na madaktari wanaogoma wanatakiwa tena mahakamani jumatano wiki hii baada ya kupewa muda wa wiki moja kurejelea mazungumzo na serikali. Kwa mara nyingine, jaji Hellen Wasilwa aliwapa maafisa hao muda zaidi wa kushauriana na maafisa wa wizara za fedha na Leba pamoja na tume ya kuratibu mishahara ya watumishi wa umma, shirikisho la waajiri na baraza la magavana kwa minjaili ya kuafikia suluhisho kuhusu matakwa ya madaktari. Mnamo ijumaa, katibu mkuu wa COTU, Francis Atwoli alijitolea kufanikisha mazungumzo hayo ili kukomesha mgomo wa madaktari uliodumu kwa miezi miwili. Jaji Wasilwa wa mahakama ya kutaua mizozo ya ajira mwezi uliopita aliwahukumu maafisa hao kifungo cha mwezi mmoja gerezani baada ua kukaidi agizo la mahakama la kufutilia mbali mgomo wa madaktari.