Wafungwa waandika historia kwa kupiga kura

Wafungwa katika magereza ya humu nchini wanapiga kura kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi wa nchi hii. Wafungwa kadhaa katika gereza kuu la Maralal katika kaunti ya Samburu waliopiga kura zao katika kituo chao cha kura nje ya kuta za gereza hilo walielezea kuridhishwa kwao kwa kuruhusiwa kutekeleza haki yao ya kidemokrasia . Takriban wafungwa elfu 55 hapa nchini wanashiriki katika uchaguzi huu mkuu huku tume huru ya uchaguzi na mipaka ikiweka mikakati ya kuhakikisha shughuli hiyo inatekelezwa katika magereza 118.

Baadhi ya wafungwa walioongea baada ya kupiga kura zao, waliwahimiza wapiga kura wote waliojisajili kujitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wanaowataka . Shirika moja lisilokuwa la kiserikali liitwalo Reformist Crime Kwetu Si Poa Engaged linaloongozwa na George Avuko, ambaye alikuwa mfungwa katika gereza kuu la kamiti, lilitoa wito kwa vijana kote nchini kupiga kura kwa busara na kujiepusha na ghasia wakati na baada ya uchaguzi.