Wafungwa Elfu Kumi Kuachiliwa Ili Kupunguza Msongamano Gerezani

Juhudi za kumaliza msongamano kwenye magereza ya hapa nchini zimezinduliwa huku lengo likiwa kupunguza idadi ya wafungwa kutoka elfu-57 hadi efu-47 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Mshirikishi wa kitaifa wa huduma kwa jamii, Atiang Mitullah alisema uamuzi wa kuwaachilia wafungwa elfu kumi wanaotumikia vifungo kufuatia makosa madogo tayari umeidhinishwa na mahakama kuu kufuatia uchunguzi wa kina wa makosa hayo.

Akiongea katika mahakama ya Embu ambapo aliongoza shughuli ya ukaguzi wa faili za wafungwa mia tatu wanaotarajiwa kunufaika na mradi huo, Mitullah alisema wale watakaoachiliwa ni wale waliohuska na uhalifu wa kiwango cha chini kama vile wizi wa vitu vidogo vidogo, unywaji pombe na wale ambao wanatumika vifungo vya nje.

Mitullha alisema baadhi wa wafungwa hao watapata ushauri nasaha ili kuwawezesha kutangamana na jamii.

Alisema machifu na manaibu wao wameshirikishwa katika mradi huo ili kuwawezesha wafungwa hao kukubalika tena katika jamii.