Wafula Chebukati aagiza kusimamishwa kazi kwa maafisa watatu wa IEBC

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC, Wafula Chebukati ameagiza kusimamishwa kazi kwa maafisa watatu wa teknolojia ya mawasiliano katika tume hiyo. Chebukati amesema kuwa mkurugenzi wa ICT James Muhati, mshirikishi Paul Mugo na afisa Boniface Wamae walihusika kwenye kasoro za kiuchaguzi baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kikatiba. Kwenye barua kwa afisa mkuu wa tume hiyo Ezra Chiloba, Chebukati amesema kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi maafisa hao watatu itarejesha imani ya umma kwa tume hiyo katika uwezo wake wa kuandaa na kuwasilisha uchaguzi wa kuaminika. Kwenye barua hiyo Chebukati amesema kuwa maafisa hao wawili wa ICT walipata haki za ziada za kufuta fomu muhimu kutoka kwenye mtambo wa tume ya IEBC kwa kutumia akaunti yake. Alisema kuwa maafisa hao watatu walishindwa kuisaidia tume hiyo kutekeleza jukumu lake kuambatana na katiba wakati wa uchaguzi huo. Iwapo Chiloba atatekeleza agizo hilo la Chebukati hii itakuwa mara ya pili ambapo Muhati amesimamishwa kazi kwenye tume hiyo. Mapema mwaka huu Muhati alitakiwa kwenda likizo ya lazima baada ya kushtumiwa kwa hujuma kufuatia ripoti za Chebukati kwamba alikataa kushirikiana kwenye ukaguzi wa mitambo ya ICT ya tume hiyo.