Wafanyikazi wa hospitali ya Machakos Level 5 wasusia kazi

Wafanyakazi wa hospitali ya Machakos Level Five walisusia kazi jana  kulalamikia mazingira duni ya kazi. Wafanyakazi hao miongoni mwao madaktari, wauguzi, wapishi na madereva miongoni mwa wengine waliandamana kutoka hospitali hiyo hadi bunge la kaunti hiyo, wakisema hawatarejea kazini hadi malalamiko yao yatakaposhughulikiwa.Walidai kuwa hospitali hiyo haina dawa na kwamba wagonjwa wanalazimika kununua dawa kwingineko.

Kadhalika walisema vifaa vingi kwenye hospitali hiyo vimeharibika na hata kusababisha kufungwa kwa vitengo vya kuwahudumia wagonjwa wa figo na wale walio na matatizo ya meno.

Akiwahutubia wafanyakazi hao nje ya majengo ya bunge la kaunti, mwanachama wa kamati ya maswala ya wafanyakazi Jeremiah Munguti alimlaumu afisa mkuu wa fedha katika kaunti hiyo kwa kuchelewa kutoa pesa za kugharamia mahitaji ya hospitali hiyo. Hata hivyo alisema mipango inafanywa kurekebisha hali hiyo.