Wafanyikazi Wa EACC Kusailiwa Upya

Wafanyikazi wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi -(EACC), watasailiwa upyaA� baada ya wasiwasi kuibuliwa kuhusu uadilifu wa maafisa hao. Mwenyekiti wa tume hiyo, Phillip Kinisu, amesema kuna haja ya kuipatia tume hiyo mamlaka ya kuwashtaki watu, iwapo itafanikiwa katika vita dhidi ya ufisadi. Kinisu alisema tume hiyo inahitaji rasilimali nyingi zaidi ili kutekeleza majukumu yake, akisema mapambano dhidi ya ufisadi yanahitaji mbinu mpya. Kinisu alikuwa akiongea alipomtembelea Spika wa bunge la Seneti, Ekwe Ethuro, ambapo walijadili wajibu wa bunge katika mapambano dhidi ya ufisadi. Kwa upande wake, Ekwe alisema taasisi zote za usalama zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja, akisema hali ya kushtumiana iliyoko sasa kati ya taaisi hizo haifai. Wakati huo huo; mkurugenzi wa mashtaka ya Umma, Keriako Tobiko, ameitisha shilingi milioni-41 chini ya bajeti ya ziada ili kuharakisha kesi za ufisadi. Tobiko anasema afisi yake huenda ikalazimika kutafuta huduma za maafisa wa nnje kwa vile haina uwezo wa kushughulikia kesi zilizoko.