Wafanyikazi kutoka nje kuendelea Kuwekewa masharti-Uhuru

Rais  Uhuru Kenyatta amekariri kuwa serikali itadumisha masharti makali  katika  utoaji wa leseni  na kuongeza muda wa leseni hizo  kwa  wafanyakazi kutoka  nje. Akiongea baada ya kufungua makao mapya  ya shirika  la kikristo la World Vision ambalo  limekuwa  likiendesha shughuli  nchini tangu  1974,  Rais alisema  mashariti makali yamewekewa utoaji wa leseni za kazi  baada ya  serikali kugundua kwamba  walaghai wamekuwa   wakitumia  vibaya fursa  hiyo. Hata Hivyo, alisema wageni wanaokuja nchini  kufanyia kazi mashirika yenye hadhi kama World Vision hawatazuiliwa kupata leseni. Huku akipongeza shirika la World Vision  kwa hatua kubwa ambazo  limepiga, Rais alitaja baadhi ya  Wakenya mashuhuri  ambao wamenufaika na shirika hilo miongoni mwao Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana  Jackson Ole Sapit,  Jaji wa mahakama ya juu  Isaac Lenaola,  Gavana wa kaunti ya Turkana Josphat Nanok, mbunge wa  Kajiado Mashariki  Peris Tobiko   na mbunge wa zamani  Lina Jebii Kilimo.