Watano washtakiwa kwa mauaji ya mwanafunzi Mombasa

Wafanyikazi watano wa shule ya chekechea ya Augustine wameshtakiwa kwa mauaji ya mvulana ya umri wa miaka-6 aliyeaga dunia baada ya kutumbukia kwenye shimo ndani ya basi la shule. Watano hao ni mwalimu mkuu wa shule hiyo, Sara Kesi, msimamizi wa maswala ya fedha ya shule hiyo, Venant Mwaliko, dereva Vald Mbadi, msaidizi wake Abdenego Mwendwa na makanika Charo Kazungu. Hata hivyo wote waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni-1 na mahakama ya Mombasa. Jaji wa mahakama kuu Dora Chepkwony aliwaagiza wafike katika afisi ya afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo kila siku na wafanyiwe uchunguzi wa kiakili. Jeremy Masila, aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya St Augustine’s Preparatory aliaga dunia baada ya kukanyangwa na gari la shule ijumaa wiki iliyopita katika eneo la Sega huko Majengo baada ya kuanguka kupitia shimo lililokuwa ndani ya basi hilo. Maafisa wa polisi walisema mtoto huyo alianguka alipojaribu kuchukua chupa yake ya maji na begi vilivyoanguka kwenye shimo la basi hilo.